Sunday, August 26, 2018

UTU 2

UTU
Utu wa mtu ni utu, hata kama hana kitu,
Kitu kwa mtu si kitu, bali utu ndio kitu,
Na utu ukifurutu, mtu huwa kweli mtu,
Utu wa mtu ni utu, katu kitu sio utu.

Mtu aliye na utu, watu humuona mtu,
Hata kama hana kitu, utu wake huwa kitu,
Kwa hiyo utu wa mtu, si kitu bali ni utu,
Utu wa mtu ni utu, katu kitu sio utu.

Kwa mtu aso na kitu, utu wake ndio kitu,
Utu hubadili mtu, aso kitu huwa mtu,
Ila aliye na kitu, hawi mtu bila utu,
Utu wa mtu ni utu, katu kitu sio utu.

Kwa mtu alo na kitu, hawi mtu pasi utu,
Utu wake huwa kutu, hata kama ana kitu,
Kitu pasipo na utu, ni sawa na ukurutu,
Utu wa mtu ni utu, katu kitu sio utu.

Kwa mtu utu ni kitu, hata kama hana kitu,
Utu ndio kila kitu, kwa mtu kuitwa mtu,
Mambo aweza kufutu, dalili zikathubutu,
Utu wa mtu ni utu, katu kitu sio utu.

Utu humfanya mtu, awe mwenye kuthubutu,
Utu waondoa kutu, sanjari na utukutu,
Utu wabadili mtu, aso mtu huwa mtu,
Utu wa mtu ni utu, katu kitu sio utu.

Tamati naenzi utu, katu simuenzi mtu,
Mola tupe watu utu, si tija kutupa kitu,
Utu ukishafurutu, mtu atapata vitu,
Utu wa mtu ni utu, katu kitu sio utu.

TAMATI


No comments:

Post a Comment